Ijumaa , 25th Mei , 2018

Klabu ya soka ya Lipuli FC imemtaja Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi Amina Amina Masenza, kuwa ndio chanzo cha mafanikio na umoja ndani ya timu hiyo inayoiwakilisha Iringa kwenye michuano ya ligi kuu soka Tanzania Bara.

Akiongea East Africa Television juu ya mwenendo wao kwa msimu mzima wa ligi kuu 2017/18, msemaji wa Lipuli FC, Clement Sanga, ameweka wazi kuwa Bi. Amina amekuwa nao bega kwa bega katika kipindi chote cha ligi kuu.

''Umoja na mshikamo wetu ndani ya klabu yetu ni matokeo ya juhudi za Mkuu wetu wa Mkoa Amina Masenza, amekuwa mtu muhimu sana kwenye kutuunganisha na kutusaidia pale tunapohitaji msaada wake hivyo mchango wake kwa timu hauelezeki'', amesema.

Mara kadhaa Bi. Amina amekuwa akitatua changamoto zilizokuwa zinaikabili timu hiyo ambayo imepanda daraja msimu huu na kuisadia kumaliza ligi katika nafasi ya 7 kwenye msimamo wa ligi kuu licha ya kusaliwa na mchezo mmoja.

Mpaka sasa Lipuli FC ina alama 38 kwenye mechi 29 ilizocheza na itamaliza ligi kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Kagera Sugar siku ya Jumatatu Mei 28, 2018.