Jumamosi , 15th Jul , 2017

Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga, amesema kikosi chake kitaivaa Rwanda (Amavubi) bila kujali rekodi ya matokeo waliyopata katika mechi zilizopita hivi karibuni kwenye michuano ya Kombe la COSAFA.

Kikosi cha Taifa Stars

Akizungumza jana, Mayanga alisema amekiandaa vyema kikosi chake kuhakikisha leo wanaanza vyema safari ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Mayanga aliendelea kusema kuwa kikubwa katika mazoezi alikuwa anawajenga wachezaji kiakili na kujipanga kutowadharau wapinzani wao ambao nao wanataka kupata matokeo mazuri ugenini.

"Tunashukuru tumemaliza mazoezi ya mwisho asubuhi hii (jana asubuhi) kazi kubwa ya benchi la ufundi lilikuwa pia kuondoa uchovu walioupata katika mechi zilizopita na pia tumewaandaa wachezaji kuikabili Rwanda bila ya kuwa na kumbukumbu ya historia ya mechi zilizopita, tunajua Rwanda ina wachezaji wenye kasi na wenye morali ya kijeshi," alisema Mayanga.

Kwa mujibu wa Mayanga kikosi chake hakina majeruhi hata mmoja, huku nahodha Himid Mao, akisema kila mchezaji amejiandaa kupambana kwa ajili ya kusaka ushindi katika mechi ya leo.