Hazard 'amzodoa' Mourinho

Tuesday , 19th Sep , 2017

Nyota wa Chelsea Eden Hazard amesema alijiona wa tofauti ndani ya wiki moja tu aliyofanya mazoezi chini ya kocha wake wa sasa Antonio Conte tofauti na hapo awali alipokuwa akifundishwa na  walimu wengine, kauli iliyotafsiriwa ni dongo kwa kocha wake

aliyepita bwana Mourinho ambaye hawakuwa na mahusiano mazuri sana na Hazard.

Hazard ameyasema hayo baada ya kuulizwa swali kuhusu urejeo wake msimu huu baada ya kuwa majeruhi akikosa mechi zote za Chelsea msimu huu.

"Najisikia vizuri kurejea na nina amini chini ya kocha wangu Conte nitakuwa bora tu kama ilivyokuwa wakati anaanza kuifundisha Chelsea, chini ya wiki moja tu nilijiona watofauti sana ukilinganisha na walimu waliopita hapa", amesema Hazard.

Hazard hakuwa na msimu mzuri wa 2015/16 chini ya Mourinho baada ya kushindwa kuanzishwa katika michezo kadhaa ambapo timu yake ilimaliza nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi na kupelekea kocha Mourinho kuondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Conte ambaye aliiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa EPL katika msimu wake wa kwanza 2016/17.

Hazard ameongeza kuwa Conte ni kocha bora amemfahamu tangu akiwa na Juventus na sasa yupo naye Chelsea na anaamini bado ana muda mrefu wa kuwa klabuni hapo.

Nyota huyo wa Ubelgji amejumuishwa kwenye kikosi cha Chelsea kitakachoshuka dimbani leo kucheza na Nottingham Forest kwenye kombe la ligi maarufu EFL Cup.