Jumamosi , 26th Mei , 2018

Waendesha magari Lewis Hamilton wa Mercedes na Sebastian Vettel wa Ferrari watalazimika kuanzisha gari zao katika nafasi ya pili na tatu, kwenye mbio za MonacoGP kesho, baada ya Daniel Ricciardo wa Red Bull kushinda nafasi ya kwanza.

Daniel Ricciardo ameongoza mbio za majaribio katika mitaa ya jiji la Monaco jioni hii, hivyo kesho kwenye mbio kuu katika mji huo, gari yake itakuwa ya kwanza akifuatiwa na Vettel aliyeshika nafasi ya pili.

Muingereza Lewis Hamilton ambaye ndio mshindi wa mbio zilizopita za Hispania katika jiji la Barcelona atapanga gari yake katika nafasi ya tatu. Nafasi ya nne imeshikiliwa na Dereva mwingine wa timu ya Ferrari Kimi Raikkonen.

Dereva mwingine wa timu ya Red Bull, Max Verstappen, amepata ajali kwenye mbio hizo za majaribio, hivyo kushindwa kuendelea lakini kampuni yake imeahidi kushughulikia gari yake ili kesho aweze kushiriki Monaco Grand Prix.

'Formula One' maarufu kama Langalanga, zipo kwenye mji wa 6 kati ya 21 ya msimu huu. Hadi sasa msimamo unaongozwa na Mercedes kupitia kwa Hamilton mwenye alama 95 akifuatiwa na timu ya Ferrari kupitia kwa Vettel mwenye alama 78.