Alhamisi , 15th Jul , 2021

Ligi ya kikapu nchini Marekani iliendelea kwa mchezo wa nne wa fainali ya ligi hiyo ambapo Milwaukee Bucks imeibuka na ushindi wa alama 109-103 dhidi ya Phoenix Suns alfajiri ya kuamkia leo Julai 15, 2021 na kufanya series kuwa na sare ya 2-2.

Devin Booker wa Phoenix Suns akijaribu kuurusha mpira ili utinge kikapuni mbele ya P.J. Tucker kwenye mchezo wa fainali ya nne dhidi ya Milwaukee Bucks alfajrii ya leo ambapo Phoenix Suns wamefungwa kwa alama 109-103.

Mchezo huo uliokuwa wa kusisimua, ulimalizika huku tuzo ya nyota wa mchezo ikienda kwa nyota wa Phoenix Suns, Devin Booker aliyekusanya alama nyingi kuliko mchezaji yeyote, alama 42 huku akicheza rebound 1 na kutoa assist 2 na kuwapiku Giannis Antetokounmpo na Khris Middleton.

Middleton alifikisha alama 40, rebound 6 na assist 4 na kushika nafasi ya pili kwa wachezaji waliokusanya alama nyingi ilhali MVP wa misimu miwili mfululizo iliyopita ya NBA, Giannis akiwa mchezaji watatu kufikisha alama nyingi, alama 26, rebound na assist 4.

Alama 42 za Booker zimemfanya aweke rekodi ya kuwa mchezaji pekee kwenye historia ya NBA kufikisha alama nyingi zaidi kwenye msimu wake wa kwanza, alama 542 na kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na mkali wa zamani San Francisco Warriors, Ricky Barry mwenye alama 521 tokea 1967.

Kwa upande wa Khris Middleton wa Bucks, ameweka rekodi yake binafsi ya kufikisha alama nyingi zaidi, alama 40 kwenye michezo ya fainali tokea aanze kucheza mchezo huo mwaka 2012.

Milwaukee Bucks itashuka dimbani kukipiga na Phoenix Suns kwenye mchezo wa tano wa fainali hiyo  Julai 18 na Julai 21 mwaka huu watacheza mchezo wake wa sita ili kumsaka mshindi wa michezo minne ambayo itatosha kumfanya awe bingwa mpya wa NBA kwa msimu wa mwaka 2020-2021.