Alhamisi , 10th Nov , 2022

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu amewataka viongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania kutafuta ufumbuzi na kuongeza umakini kuhakikisha nidhamu inaimarika zaidi katika mchezo wa soka.

Rai hiyo ameitoa leo tarehe 10 Novemba, 2022 alipokuwa anafungua mkutano mkuu wa 9 wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) uliofanyika katika ukumbi wa Jengo la NSSF Ilala jijini Dar es Salaam.

"Utafutwe ufumbuzi zaidi na kuongeza umakini, kuhakikisha nidhamu inakuwa kubwa ili soka letu liwe kioo dhidi ya nchi nyingine, yapunguzwe matukio ya kuondoa sintofahamu kwa wadau wa soka ndani na nje ya nchi," amesema Yakubu.

Aidha Yakubu amewataka wachezaji, viongozi wa ngazi zote na makocha kuzingatia kanuni zilizopo ili kuondokana na matukio yasiyofaa katika michezo nchini.

"Siamini kujengwa kwa magereza mengi ndio suluhisho la kuondoa vibaka wengi mtaani, bali ni kutoa elimu ya kuwafanya waondokane na nidhamu mbovu, hivyo nitoe wito kwa wachezaji, viongozi wa ngazi zote na makocha wazingatie kanuni zilizopo kwa lengo la kuondoa matukio yasiyofaa," amesema  Yakubu.