Ijumaa , 11th Aug , 2017

Mechi ya kirafiki ya Mabingwa wa ligi Kuu bara Yanga SC dhidi ya Ruvu Shooting iliyokuwa ichezwe kesho kwenye Uwanja wa Taifa imehamishwa na sasa itachezwa Uwanja wa Chamazi kutokana na Uwanja wa Taifa  kesho kutumika kwa shughuli za kiserikali.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ametoa taarifa hiyo na kusema mechi hiyo imehamishiwa Chamazi ilikupisha shughuli hizo

"Tumepata taarifa  kutoka serikalini asubuhi kuwa Uwanja wa Taifa  kesho unatumika kwa shughuli za kitaifa hivyo hatutaweza kucheza mechi yetu hapo na kama unavyojua hatuwezi kubishana na Serikali. Tunaishukuru Azam kwa kutukubalia mechi yetu tuihamishie kwenye uwanja wao, hivyo tunawaomba mashabiki waje kwa wingi Chamazi kushuhudia mchezo huo kama walivyofanya katika mchezowa awali ambapo viingilio vitakuwa Sh7,000 kwa VIP na Sh 5,000 mzunguko." alisema Mkwasa.

 Mkwasa alisema baada ya mchezo huo wa kesho, Yanga itaondoka Jumapili asubuhi kwenda Zanzibar na usiku itacheza mechi nyingine ya kirafiki  na Mlandege  itakayofanyika kwenye Uwanja wa Aman na baadaye kuelekea Pemba kujifua kwa ajili ya mechi ya  Ngao ya Jamii dhidi ya Simba itakayofanyika Agosti 23.