Jumamosi , 18th Sep , 2021

Kocha Mkuu wa klabu ya Arsenal 'Washika mitutu wa jiji la London', Mikel Arteta amefunguka na kusema anaumia sana kuona wapinzani wake wanashiriki michuano ya klabu bingwa Ulaya muda ambao Arsenal imetimiza miaka minne mfululizo bila kushiriki michuano hiyo.

Picha ya kocha Mikel Arteta

Arteta amesema "Unaniumiza sana, siku chache zilizopita nilivyowasha Luninga na kuona timu nyingine zikishiriki michuano hiyo na sio Arsenal".

Arteta ameyasema hayo akiwa anazingumza na Wanahabari kuelekea mchezo wake wa EPL ugenini dhidi ya Burnley utakaochezwa Saa 11:00 Jioni ya leo Septemba 18, 2021 kwenye dimba la Burnley la 'Turf Mor'.

Kuelekea kwenye mchezo huo, Arsenal itawakosa nyota wake watatu kutokana na sababu mbalimbali, Nyota hao ni Granit Xhaka anayetumikia adhabu ya kuoneshwa kadi nyekundu, Mohammed Elneny anayesumbuliwa maumivu ya Misuli ilhali Rob Holding anamaumivu ya goti.

Kwa upande wa Burnley, kocha wake Sean Dyche amesema hatomuharakisha kumchezesha mchezaji wake mpya Maxwel Cornet licha ya kuwa na mchezo huo ni  mkubwa mbele yake.

 Sean ataingia kwenye mchezo huo akiwa na ari nzuri baada ya kusaini kandarasi ya miaka 4 kusalia Turf Mor hadi mwaka 2025 huku akiwa kocha aliyehudumu EPL kwa muda kulinganisha na makocha waliopo sasa, muda wa miaka 9.

Arsenal ambayo haijamfunga Burnley kwenye michezo mitatu ya mwisho, ipo nafasi ya 17 ikiwa na alama 3 baada ya kucheza michezo 4 ilhali Burnley ipo nafasi ya 19 wakiwa na alama 1 licha ya kucheza michezo 4.