Kukwama biashara ya Wema, sababu yaanikwa

Monday , 18th Sep , 2017

Meneja wa msanii gumzo bongo Wema Sepetu, amefunguka kuhusu tetesi za bidhaa ya lipstick ya msanii huyo 'Kiss by Wema' kuzuiwa kuingia sokoni kutokana na ubora, na kusema kwamba taarifa hizo hazina ukweli.

Akizungumza na mwandishi wa habari wa East Africa Television meneja huyo aliyejulikana kwa jina la Happy Shame, amesema mzigo huo haupo sokoni kwa sababu msimu wa kuingiza mzigo mpya bado, na sio kama umezuiwa na serikali kutokana na ubora.

"Hicho kitu sijasikia wala sijatumiwa 'email' kuambiwa kwamba lipstick zimezuiwa, hivi vitu vinaenda na msimu, muda wake ukifika tutaziachia, kwa hiyo hakuna ukweli isipokuwa kuna baadhi ya vitu tunavikamilisha baadaye mzigo utatoka", amesema Happy Shame.

Hivi karibuni kumekuwa na tetesi kwamba 'lipstick' hizo zimezuiwa kuingia nchini kwa sababu hazijakidhi ubora na kwamba ndio sababu ya kutopatikana mtaani kama ambavyo zilikuwa zikigombaniwa, jambo ambalo limepigwa na Meneja wa Wema Sepetu. 

Bidhaa ya Lipstick za 'Kiss by Wema' za Wema Sepetu