'Kazi yake Mola' nilituliza kichwa - Madee

Thursday , 18th May , 2017

Madee Seneda amefunguka na kudai siri ya wimbo wa kazi yake mola kufanya vizuri mpaka sasa ni kutokana na kutuliza kichwa wakati anaandika mashairi yake tofauti na vijana wa sasa ambao wanaingia studio wakiwa hawajui wanataka kuimba nini.

Jana akiwa kwenye Planet Bongo ya East Africa radio, Madee amesema kuwa pamoja na kuwa zimeimbwa nyimbo nyingi zenye mahadhi ya maombolezo lakini 'Kazi yake Mola' bado imeendelea kuwa wimbo bora kutoka na mashahiri kupangiliwa kwa ubunifu wa hali juu ikiwa ni pamoja na 'beat' ya P. Funk Majani.

"Kazi yake Mola P. Funk aliitengenezea beat ambalo mpaka sasa limeweza kudumu, lakini pia mashairi niliyaandika kwa umakini mkubwa kwani ndo nilikuwa nimepatiwa nafasi ya kuonyesha uwezo wangu. Japo wimbo haukuwa wa kutoka officially lakini nilijitahidi kuandika mashairi yenye maudhui, ndio maana mpaka sasa wimbo unaonekana hit. Vijana wa sasa wameshindwa kutoa nyimbo itakayoizidi 'kazi yake mola' kwani wengine mpaka wanaingia studio hawana hata mashairi wanataka wasikie mdundo ndio wapate kitu cha kusema"- Madee.

Aidha Madee ameongeza kutokana na ubora wa kazi yake mola amewaomba mashabiki zake kuendelee kuutumia katika maombolezo ya ndugu, jamaa na marafiki akiwepo Msanii aliyetamba na wimbo ya Kazi yangu ya dukani, Dogo Mfaume aliyefariki dunia mapema jana.