Jumanne , 31st Oct , 2017

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe, amekamatwa na Jeshi la Polisi asubuhi hii akiwa nyumbani kwake jijini Dar es salaam  na amepelekwa kituo cha Polisi Chang'ombe.

Taarifa fupi iliyotolewa na Afisa habari wa Chama hicho Abdallah Khamis, amethibitisha kukamatwa kwa kiongozi huyo huku akibainisha kwamba sababu za kukamatwa kwake zinawezekana kuwa ni kutokana na hotuba yake aliyoitoa juzi Oktoba 29, 2017 katika kata ya Kijichi, Mbagala Jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 43 nchini.

Taarifa zilizotolewa na Kamati ya Sheria na Katiba ya ACT imedai kwamba sababu za kukamatwa kwa  Mh. Kabwe Zitto kabwe zimehusishwa na tuhuma za uchochezi na kwamba imedaiwa kuwa alipokuwa kwenye mkutano wa kuzindua kampeni za udiwani katika Kata ya Kijichi, Wilayani Temeke alitoa maneno yanayoweza kupelekea uvunjifu wa amani ambapo maneno hayo ni kama yafuatayo :

"Kwamba wananchi wasiichague CCM kwa sababu Serikali yake imeshindwa kufanya uchunguzi na kuwakamata watu waliompiga risasi Mbunge Tundu Lissu mpaka siku hiyo".

Imeongezwa kwamba Bw. Zitto amesema "Kwamba wananchi wasiichague CCM kwa sababu Serikali yake imeshindwa kueleza chanzo cha miili ya watu wanaookotwa kwenye fukwe za bahari kama Coco Beach. Hivyo kuichagua CCM ni sawa na kuwaunga mkono waliofanya vitendo vya kumshambulia Tundu Lissu na wanaoua watu wanaookotwa kwenye fukwe".

Hata hivyo Timu ya mawakili wa chama iko na ndugu Zitto katika mahojiano hayo.

UPDATE Mbunge Zitto amekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi Kamata, Baada ya kuachiwa katika kituo cha polisi cha Chang'ombe kwa dhamana.