Alhamisi , 15th Jul , 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Dkt. Saada Mkuya Salum amezitaka mamlaka husika kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika na kupoteza vielelzo vya madawa katika mamlaka zenye dhamana ya madawa ya kulevya.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Dkt. Saada Mkuya Salum

Kauli hiyo imekuja kufuatia kutokuridhishwa na utunzaji wa vielelezo hivyo katika Mahakama na Polisi Kisiwani Pemba jambo ambalo ameeleza kuwa linaweza kuwa ndiyo kikwazo kwa kesi nyingi za madawa kuondoshwa Mahakamani bila ya watuhumiwa kupewa adhabu.

“Kete 4763 za heroin tumetafuta vielelezo hatujaziona lakini hili hatutoliachia hapa kwa sababu tumeona kumekuwa na mapungufu mkubwa sana ya usimamizi kesi nyingi za heroin zimeachiwa lakini hata uhifadhi wa vielelezo hatutaachia hivi hata hao ambao wamehusika kwa namna moja au nyingine kupoteza hivyo vielelezo basi watawajibika katika hili,” amesema Dkt. Saada.

“Lakini kwa hali hii na vielelzo hivi tunapimaje kama huu unga umerudi mtaani hatuna uhakika sisi tunalaumiwa kwamba hatufanyi kazi kumbe uzembe uko kwa watendaji wenu,” amesema Luteni Kanali Burhan Zubeir Nassor Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Zanzibar.

Nayo Kamati ya Uteketezaji Madawa ya Kulevya Zanzibar imesema haijaridhishwa na namna ya utunzaji wa vielelezo vya madawa katika mamlaka zenye dhamana hizo Kisiwani Pemba jambo ambalo linaweza kutoa mwanya kwa madawa hayo yaliyokamatwa kurudi kwa watumiaji mitaani.

Kwa upande wake Mrajisi wa Mahakama Zanzibar Mohamed Ali Mohamed ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo ametaka kamati kuchukua hatua stahiki juu ya mapungufu yaliyojitokeza na Mahakama nayo itachukua hatua kwa wale waliozembea majukumu yao.