Heche kupeleka hoja binafsi muda Urais upunguzwe

Monday , 18th Sep , 2017

Mbunge wa Tarime Vijijini kupitia  (CHADEMA) John Heche amefunguka na kusema anakusudia kuwasilisha bungeni hoja binafsi ili kupunguza muda wa viongozi kukaa madarakani kutoka miaka mitano na iwe miaka minne kama Marekani.

John Heche amesema hayo leo kupitia mitandao yake ya kijamii zikiwa zimepita siku kadhaa toka Mbunge wa Chemba Mhe. Juma Nkamia (CCM) kusema anatarajiwa kuwasilisha muswada binafsi bungeni kulitaka bunge kufanya marekebisho ya katiba ili viongozi waweze kukaa miaka saba. Jambo ambalo Heche anapinga na kusema kuwa muda ambao viongozi wanakaa madarakani ni mkubwa sana.   

"Nakusudia kuwasilisha bungeni hoja binafsi kupunguza muda wa kukaa madarakani kwa Rais, wabunge na madiwani kutoka miaka 5 mpaka 4 tuwe kama Marekani ili kutoa nafasi kwa wananchi kuwa na maamuzi zaidi kuhusu uendeshaji wa nchi yao" Alisema John Heche 

Aidha John Heche amesema kuwa kiongozi akikaa madarakani muda mrefu anajisahau na kuona ile nafasi kama ni yake pekee yake jambo ambalo si sawa hata kidogo 

"ukikaa sana madarakani unafikiri nchi ni mali yako, kuna viongozi wengi sana wazuri ila hawajapata muda tu wa kuongoza" alisisitiza John Heche.