Jumatano , 25th Mei , 2022

Mbunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuja na Mipango kabambe ambayo itaboresha sekta hiyo ili iweze kuzalisha ajira kwa wingi kama ilivyokua miaka ya nyuma.

Mbunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile

Ditopile ametoa kauli hiyo leo wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Bungeni jijini Dodoma.

"Mwaka 2014/15 Tanzania tulia tunatoa tani zaidi ya 45,000 ya minofu ya Sangara na mazao yake,lakini mwaka 2021 tumetoa tani 41,000 tu, Niwe mkweli hali ya Sangara katika Ziwa Viktoria imekua mbaya Sana sijui kama Waziri hili jambo mmeliona na kulitafutia ufumbuzi.

Ukienda kuwahoji wanachinga wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa wengi walikua waajiriwa katika Viwanda vinavyochakata mazao ya Uvuvi, Viwanda hivyo kwa sasa vimepunguza uzalishaji tukumbuke mapato yaliyokua yanapatikana kupitia Sangara yaliyokua yanaleta maendeleo nchini," Amesema Ditopile.

Amemtaka Waziri wa Uvuvi Mashimba Ndaki kuja na majibu ya msingi yanayoonesha namna gani kama Wizara wamejipanga kuhakikisha wananyanyua sekta ya Uvuvi nchini ili kuweza kuipatia Nchi mapato makubwa lakini pia kusaidia kupunguza changamoto ya ajira kupitia Uvuvi.