Ijumaa , 25th Mei , 2018

Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Ahmadi ameliomba Bunge kuchukua hatua kali dhidi ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa kutokutoa fedha zinazopitishwa na mhimili huo.

Katani amesema miradi mingi imekuwa ikishindwa kutekelezwa kutokana na wizara ya fedha kushindwa kutoa fedha licha ya Bunge kuzipitisha.

Amesema wakandarasi wa Rea wameshindwa kutekeleza usambazaji wa umeme kwa kukosa fedha ambazo zilipitishwa na Bunge huku mawaziri wakinyooshewa vidole kwa makosa ambayo si ya kwao.

“Sijui wizara ya fedha tufanye jambo gani, tumeona katika kilimo, fedha za korosho hakuna sijui kuna jinsi gani wizara ya fedha,” ameongeza

Katani amesema hakuna mpinzani nchini si mzalendo au kupinga miradi yenye tija kwa taifa lakini wanayozungumza Serikali inapaswa kuyasikiliza na kuyafanyia kazi.

Sisi sote ni wazalendo tunachokisema mtumie hekima za pamoja, mawaziri msikilize yanayosemwa, kama haya mnaambiwa katika Stiegler’s Gorge mkubali tunayosema, kwamba tathimini iko wapi, ilifanyika lini,  tukisema mnasema sio wazalendo, Tunaposhauri tunashauri na nia nzuri, hatuna tatizo na CCM, tuna tatizo na matendo ya CCM, tukisema mnaanza kusema nini,” amesema Katani