Jumamosi , 24th Sep , 2016

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi ,Utumishi na Utawala Bora Mhe. Suleiman Jafo amewataka wadau mbalimbali kuisaidia Serikali katika utatuzi wa changamoto ya Majengo na Vifaa vya maabara ili kuleta matokeo mazuri katika sekta ya elimu nchini.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya kupokea madawati 1200 yenye dhamani ya shilingi Milioni 147 Mhe, Jafo amesema licha ya kufanikiwa kumaliza uhaba wa madawati kwa asilimia 80 lakini suala la majengo, vyumba vya madarasa na vifaa vya maabara bado ni changamoto.

Mhe. Jafo amesema madawati hayo yatapelekwa kwenye shule zenye uhitaji mkubwa wa Madawati zilizopo Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma na Mkoa wa Shinyanga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Degratius Ndejembi amesema msaada huo katika Wialaya yake utatatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya Madawati na ameshukuru kampuni za Geita Gold Mine na makampuni mengine yaliyowapatia msaada huo wenye lengo la kuinua kiwango cha elimu katika Wialaya yake.

Naye Afisa Mawasiliano kutoka kampuni ya Uchimbaji madini ya Geita Gold Minging (GGM )Tenga Tenga ameeleza kuwa kampuni hiyo haijajikita kuchangia madawati pekee bali lengo lake ni kuhakikisha inaisaidia serikali ya Tanzania kutatua changamoto za kielimu kama vile kununua vifaa mbalimbali vya kufundishia wanafunzi zikiwemo komputa ili kuweza kuifanya Tanzania kuwa na elimu bora na yenye viwango.