Jumapili , 15th Mei , 2022

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amewataka wadau wa tasnia ya Kuku nchini kutafakari namna ya kupunguza gharama za uzalishaji ili mnufaika wa mwisho ambaye ni mlaji aweze kununua Kuku kwa bei nafuu na kufikia lengo la kila Mtanzania kula nyama kilogramu 50 kwa mwaka.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki.

Amebainisha hayo jijini Dar es Salaam, na kufafanua kuwa wazalishaji wa chakula cha Kuku wanatakiwa kutafakari namna ya kupunguza bei za vyakula vya kuku hali kadhalika wazalishaji wa vifaranga vya kuku kupunguza bei za vifaranga ili watu wengi wajitokeze kufuga kuku na kufanya bidhaa hiyo upatikanaji wake uwe wa wingi na bei nafuu.

Waziri Ndaki amesema endapo bei za vyakula vya Kuku na vifaranga zitazidi kupanda, mnufaika wa mwisho hataweza kumudu kununua kuku ambapo amesema kwa sasa ulaji wa nyama hapa nchini kwa kila mtanzania ni takriban kilogramu 15 kwa mwaka kulingana na utafiti uliofanywa na FAO.