Waziri ataka misingi ya Nyerere

Wednesday , 11th Oct , 2017

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. William Ole Nasha amewataka Watanzania kurejesha nchi katika misingi iliyoachwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Rai hiyo ameitoa leo jijini Dar es salaam wakati akifungua Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 18 ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Naibu Waziri Ole Nasha ameeleza kuwa Hayati Baba wa Taifa alisisitiza zaidi nchi kuwa na viongozi waadilifu,wazalendo na wenye uchungu na nchi yao.

Aidha Ole Nasha amesema sikuhizi kumekuwa na wimbi kubwa la kuporomoka kwa maadili, kushamiri kwa rushwa, ufisadi, pamoja na kukosekana kwa uzalendo na uwajibikaji miongoni mwa Watanzania.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa ili kufikia malengo kwenye uchumi wa viwanda ni lazima kuzingatia Uzalendo, Utaifa, Uadilifu na Uongozi Bora.