Alhamisi , 24th Mei , 2018

Wazazi wawili mjini New York wameshinda kesi waliyokuwa wakipambana kumfukuza nyumbani kijana wao mwenye umri wa miaka 30 baada ya kukaidi kuondoka.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo katika mahakama ya juu ya jimboni humo, Jaji Donald Greenwood ameamuru kijana huyo aondoke nyumbani kwa wazazi wake.

Jaji Greenwood alimwambia kijana huyo kuendelea kubaki nyumbani kwa miezi sita zaidi kama alivyoomba 'haikubaliki.

Walipokuwa wakifungua mashtaka juma lililopita,Christina and Mark Rotondo walionyesha nakala ya nyaraka walizokuwa wakimuamuru kuondoka nyumbani tangu tarehe 2 mwezi Februari mwaka 2018.

Aidha wazazi hao walimpatia dola za Marekani 1,100 ili aondoke nyumbani, kwa mujibu wa barua walimtaka auze baadhi ya vitu vyake ikiwemo gari yake mbovu aina ya Volkswagen Passat.

Kijana Michael Rotondo ambaye alijiwakilisha mwenyewe mahakamani, amesema ''Sijui kwa nini hawawezi kusubiri kidogo kabla ya mimi kuondoka", Bwana Rotondo alieleza huku wazazi wakiwa wamekaa karibu na mwanasheria wao wakimtazama.

Ameongeza kuwa miezi sita ndio muda uli sahihi kwa mtu ambaye alikuwa akiwategemea watu .
Pamoja na hayo Bw. Michael Rotondo aliwaambia waandishi wa habari kuwa atakata rufaa, na amepanga kuondoka nyumbani miezi mitatu ijayo.