Ijumaa , 18th Mei , 2018

Mbunge wa kuteuliwa AbdallaH Bulembo amemtaka Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, kuunda Tume maalumu ya Bunge ambayo itachunguza  madhara  waliyopata wananchi kutokana operesheni mbalimbali za kuzuia uvuvi haramu nchini.

Bulembo amesema hayo leo Mei 18, 2018 Bungeni mjini Dodoma alipokuwa anachangia hoja ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya mifugo na uvuvi katika mwaka wa fedha 2018/2019 na kuongeza kuwa wananchi wamekuwa watumwa katika nchi yao kutokana na kunyanyasika na operesheni hizo.

“Baada ya miezi tisa mnaenda kuomba kura kwenye serikali za mitaa, mnaenda kusema nini kwa hali hii? mnaendaje kuongea na watu hawa? mtanzania anakuaje mtumwa kwenye nchi yake? wafanyakazi wanalia, wafanyabiashara wanalia, watu wote wanalia inawezekanaje, Mpina huwatendei haki watanzania na hii kuna siku Mungu atahukumu, watu wamekuwa watumwa kwenye nchi yao kwasababu ya kuvua” amesema Bulembo.

Mbunge huyo ameongeza kuwa Waziri wa mifugo na uvuv Luhaga Mpina amekua kiongozi asiyependa kusikiliza shida wanazopata wananchi kutokana na uendeshwaji mbovu wa operesheni hizo, Bulembo amesema “wafugaji wanadhambi gani, kufuga ni dhambi? waziri anafuatwa mpaka kwenye viwanja vya Bunge hataki kuwasilikiza watu, wewe ni waziri wa nani? kama hauwahudumii watu uwaziri wako ni wa nini?”

Bulembo amedai kwamba hataunga mkono hoja ya Wizara Mifugo ya Uvuvi mpaka pale itakapoundwa Tume na waziri husika kusimamisha operesheni kwani katika operesheni hizo wapo baadhi ya watu ambao walipigwa risasi na wengine kujinyonga.