Alhamisi , 8th Jul , 2021

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Khamis, ameagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi watatu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa wanaodaiwa kushirikiana na mawakala wa Benki kuchepusha takribani shilingi mil. 20 kwa ajili ya ununuzi wa dawa.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na kupokelewa na Viongozi waandamizi ya Hospitali hiyo kwa ziara ya kikazi.

Mhe. Mwanaidi ametoa agizo hilo katika kikao na watendaji waandamizi wa Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake Mkoani Iringa, na kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa katika hospitali hivyo hatofumbia macho vitendo vyovyote vya ubadhirifu wa fedha za umma.

“Nimesikia taarifa ya hospitali lakini nahoji, sikusikia taarifa za upotevu wa fedha za Hospitali kupitia akaunti za watumishi wa hapa au sio Hospitali hii?, niseme hatuwezi kuvumilia haya madudu kabisa fedha zinatolewa na Serikali kuja kutoa huduma kwa wananchi wewe mtumishi wa umma unajimilikisha hili hapana tunashughulika nalo,” alisema Niabu Waziri Mwanaidi.
 
Aidha, Naibu Waziri Mwanaidi ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kuhakikisha wanasimamia kwa ukamilifu matumizi ya fedha zinazoletwa na Serikali kwa malengo ya kutoa huduma kwa wananchi na sio kujifunaisha watu wachache. 
 
Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Abbas Idd amesema ni kweli tukio hilo limetokea na linafanyiwa kazi na vyombo vya uchunguzi ili kubaini wale wote waliohusika na kuweza kuwachukulia hatua.
 
“Mheshimiwa Naibu Waziri kulikuwa na matukio mawili tofauti lakini kama ni suala hilo, kweli kuna baadhi ya wafanyakazi wenzetu wamebainika kushirikiana na baadhi ya mawakala wa Benki na kuhamisha fedha za malipo ya dawa kwenda kwenye akaunti zao binafsi,” alisema Abbas.
 
Baada ya maelezo hayo, Mhe. Mwanaidi akaagiza kudhibitiwa kwa akaunti za watumishi na mawakala wa Benki waliohusika na kuhakikisha kwamba uchunguzi wa kina unafanyika ili kuepusha udanganyifu wa aina hiyo kuendelea kutokea na Mawakala wa Benki walioshirikiana na watumishi wa Hospitali hiyo kuchepusha fedha za umma kulipa fedha hizo ili kufidia hasara iliyopatikana.