Jumatano , 30th Nov , 2022

Katika kipindi cha miezi 10 halmashauri ya wilaya ya Geita imepokea taarifa 26 za vitendo vya ukatili kwa wanawake na Watoto, huku ikiwaomba wanaume kutoa taarifa kwani wengi wao wamekuwa wakiona aibu kutoa taarifa hizo na kusababisha kukosa takwimu sahihi ya ukatili wanaofanyiwa

Hayo yamesemwa na afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Geita kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili zenye kauli mbiu ya kila uhai una thamani huku baadhi ya waume wakielezea sababu za wao kutopata sauti zao

"Matukio ya Ukatili yaliyotolewa taarifa ni 26, katika natukio hayo, ubakaji yamikuwa ni saba, ulawiti wawili na vipigo ni 17, mheshimiwa mgeni rasmi, pamoja na matukio hayo kutolewa taarifa na wanawake na watoto, lakini pia wanaume baadhi wamekuwa ni wahanga wa Ukatili japokuwa hawatoi taarifa katika ofisi zetu na hivyo kukosa takwimu zao kwa urahisi", alisema Mwanakatwe

"Sisi kama wanaume tunafanyiwa sana ukatili wa kijinsia na wanawake yani wake zetu lakini unashindwa kuanzia kwamba uende wapi kwa sababu sisi huwaga hawatujali sana, mnaowajali sana ni wanawake, sasa ninashindwa kuelewa labda kwa siku ya leo kwakuwa waandishi mmekuja mimi lazima nitoe tu ya ukweli hata sisi tunateswa sana", alisema Mashiri

Msimamizi wa maswala ya kijinsia kutoka shirika la Plan International Hildegada Mashauri amewaomba wananchi kutoa taarifa za Ukatili ili jamii itakapoona watuhumiwa wamechukuliwa hatua itapunguza vitendo hivyo

"Vitendo vyote vya Ukatili wa kijinsia wakatoe taarifa kuna dawati la Jinsia lakini tuna kamati za MTAKUWA ambazo zipo kwenye vijiji na kwenye kata kwahiyo mtu atakapopitia au atakapofanyiwa unyanyasaji wa aina yeyote aende akaripoti, tunaporipoti au tunapokuwa tunatoa taarifa tuna Imani kwamba, yule aliefanya kitendo cha Ukatili jamii ikiona sheria imechukuliwa hivi vitendo vitaweza kupungua kwa kiasi kikubwa", alisema Mashauri. 

Mkuu wa wilaya ya Geita Wilson Shimo, amewataka wananchi na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoishia kwenye siku16 za kupinga Ukatili badala yake wafanye kama mtindo wao wa Maisha ili kuepusha vitendo vya ukatili vilivyokithiri wilayani humo

"Siku hizi 16 za kuonesha namna gani  tunapinga Ukatili zisiishie tu ndani ya kipindi hiki, iwe ni sehemu yetu ya kuishi, iwe ni sehemu ya maisha yetu ya kupambana na kutokomeza Ukatili ambao upo ndani ya jamii yetu", alisema Shimo.