Alhamisi , 1st Dec , 2022

Jamii ya watu wanaojitambua kuishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI wilaya ya Tabora wametakiwa kuacha kutumia vishawishi ikiwemo kuwadanganyia fedha vijana wadogo na hatimaye kuwapa maambukizi kwa makusudi.

Wadau wa UKIMWI mkoa wa Tabora

Katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo kwa wilaya ya Tabora yamefanyika viwanja vya shule ya msingi Kapunze, Kata ya Ikomwa, wadau wa mapambano dhidi ya  maambukizi ya virusi vya  UKIMWI  wilayani Tabora,wakati wakitoa salamu katika maadhimisho hayo wamesema wapo watu wenye fedha wakiwemo akinamama wenye umri mkubwa wamekuwa wakiwalaghai vijana kwa fedha na hatimaye kuwatumbukiza katika maambukizi ya UKIMWI.

Akizungumza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Ramadhani Kapela, ambaye ndiye mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amesema kitendo hicho sio cha kiungwana huku akitoa rai kwa jamii pia kuacha kuwanyanyapaa watu wenye maambukizi ya VVU.

Wakati Dunia ikiadhimisha siku ya UKIMWI hii leo Desemba Mosi, 2022, Mratibu wa UKIMWI katika Manispaa ya Tabora Aziza Mgeta, ametaja maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa wilaya ya Tabora kupungua kutoka 5% mpaka 3.8% kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2019.