Jumanne , 19th Jun , 2018

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limesema litaunda tume maalum kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha ajali ya gari la Igunga Trans lililoua watu 13, wakiwemo vijana 10 wa JKT, askari mmoja wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na raia wawili iliyotokea eneo la Igodima jijini Mbeya.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Martin Busungu

Akizungumza wakati wa zoezi la kuaga miili ya askari hao lililofanyika katika viwanja vya JKT Itende Mbeya, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini Martin Busungu, amesema mara baada ya tume kukamilisha uchunguzi wa ajali hiyo hatua kisheria zitachukuliwa kwa yeyote aliyehusika.

Akitoa salama za pole kwa ndugu na Taifa kwa ujumla kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Venance Mabeyo, Mnadhimu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni  Jenerali Yakoub Mohammed amesema taifa litawakumbuka vijana hao kwa uzalendo ikiwemo ujenzi wa ukuta wa Mererani, na kuongeza kuwa vijana waliopata ulemavu wa kudumu katika ajali hiyo Jeshi litaandaa utaratibu wa namna ya kuwasaidia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Paul Ntinika kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Amos Makalla,  amewataka watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali zinazoweza kuepukika.