Jumatatu , 22nd Nov , 2021

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameagiza Wakuu wa Wilaya za mkoa huo kuhakikisha wanafuatilia na kudhibiti kuongezeka kwa wanafunzi wa kike wanaokatisha masomo kutokana na tatizo la mimba ambapo kwa mwaka 2021 matukio 25 ya wanafunzi wa kike kupewa mimba yameripotiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti akiongea na wanafunzi wa shule ya sekondari Kirando wilaya ya Nkasi kwenye moja ya ziara zake kuhamasisha elimu.

Akizungumza mjini Sumbawanga Mkuu huyo wa Mkoa alionesha kutofurahishwa na kasi ya kuongezeka kwa wanafunzi wa kike wanaoshindwa kukamilisha masomo yao sababu ikitajwa kuwa ni kupata ujauzito.

“Lazima tuongeze mapambano kudhibiti mimba za utotoni .Sijafurahishwa kuona wilaya ya Nkasi ikiwa na idadi ya wanafunzi Ishirini Tano (25) mwaka huu waliopata mimba wakiwa wanasoma. Hii haikubaliki. Wakuu wa wilaya nendeni mkadhibiti vitendo hivi” alisisitiza Mkirikiti.

Takwimu za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa zimeonesha kuwa katika mwaka huu 2021 wilaya ya Nkasi imekuwa na matukio 25 ya wanafunzi wa kike kupata mimba huku wilaya ya Kalambo ikiripoti wasichana wanane (8) na Wilaya ya Sumbawanga nayo ikiwa na wanafunzi wanane (8).