Ijumaa , 24th Jun , 2022

Wakazi  wapya wa kijiji cha Msomera, Handeni Mkoani Tanga waliohamia kutoka Ngorongoro wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya huduma za jamii katika eneo hilo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza, Bw. Richard Tobiko Ole Makoro (kulia) ambaye ni mmoja wa wakazi wapya wa kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoa wa Tanga waliohamia katika kijiji hicho kutoka Ngorongoro wakati alipofika nyumbani kwa mkazi huyo kujionea mazingira anayoishi, Juni 23, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Hayo yameelezwa na baadhi ya wakazi hao mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea eneo hilo jana Juni 23, 2022 kukagua makazi na miundombinu ya huduma za jamii inayojengwa katika eneo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mkazi mpya wa kijiji hicho Bw. Richard Tobiko Ole Mokoro alisema kuwa yaliyofanyika katika kijiji hicho ni upendeleo wa kutosha ambao hawakuutegemea.

“Kwa fidia tu ambayo tumeipata, hata kama mtu asingepewa hivi vitu tulivyopewa na Mhe. Rais wetu Samia Suluhu Hassan asingelalamika, tunamuomba atakapopata nafasi aje hapa Msomera ili tuweze kumshukuru wenyewe.”

Alisema kuwa huduma ya maji katika eneo hilo ni ya kutosha na kuna vituo vya kuchotea maji kila baada ya mita 400 vinafungwa. “Kwa sasa kuna maboza yanaleta maji tena ni maji mazuri ambayo hata wenyeji tuliowakuta wanayasifia mno hawakuwa nayo hapo awali.”

“Kule Ngorongoro tulikuwa tunanywesha ng'ombe inapita siku moja hunyweshi, lakini huku tumekuta maji ni mengi kila siku wanakunywa maji.”

“Tunamshukuru sana Rais Samia, sasa tumepata uhuru, tumepata hatma ya maisha yetu, kwa sasa mtu unaweza kufanya chochote ambacho unataka kufanya, tofauti na ilivyokuwa Ngorongoro.”

Aliongeza kuwa anaamini katika kipindi cha miezi mitatu, kijiji cha Msomera kitakuwa kikubwa hasa kutokana na huduma ambazo zinaendelea kupelekwa na Serikali. “Siipatii picha Msomera itakuwaje. Huduma ni nyingi sana zinazoletwa na Serikali.”

Kwa upande wake, Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa idadi ya wananchi wanaojiandikisha kuhamia katika eneo hilo imeendelea kuongezeka siku hadi siku. “Serikali yenu ni aminifu, wakati tunaanza kutekeleza hili watu hawakuwa wanaamini na ninyi mnajua upendo aliokuwa nao Mheshimiwa Rais  wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kuja kuwahudumia.”

“Mlipokuja hapa mmeona wenyewe, mmepata nyumba pamoja na hati, shule ya msingi na Sekondari ipo hapa, miradi ya maji inajengwa, tunajenga barabara, tunajenga kituo cha afya, huduma hizi ni za wote.”
Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza wajenzi wa nyumba katika kijiji cha Msomera kwa kutekeleza zoezi hilo kwa viwango na kasi kubwa. “Tuliweka malengo ya kujenga nyumba 103 na zote tayari zimekamilika na ujenzi wa nyumba nyingine zilizobaki ili kufikia idadi ya nyumba 500 unaendelea.”

Naye, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. David Silinde alisema kuwa katika eneo hilo Serikali imejenga shule mpya ya msingi na nyingine imekarabatiwa. "Tunajenga nyumba za walimu, mabweni, shule mpya ya sekondari imekamilika pia tunajenga kituo cha afya na fedha ipo.”

Awamu ya pili ya zoezi la kuhamisha wakazi wa eneo la Ngorongoro kwa hiari lilianza tarehe 20.06.2022 ambapo jumla ya kaya 27 yenye watu 127 na mifugo 488 watahamisha, kaya 1 kati hizo itahamia Karatu.