Alhamisi , 24th Mei , 2018

Wakili wa utetezi katika kesi inayowakabili Harbinder Seth na James Rugemalira, ameutaka upande wa mashtaka ufanye kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na Katiba kwa kujali haki za washtakiwa ili kesi iendelee na kwamba ndani ya siku 14 ueleze upelelezi umekamilika, kama haujakamilika;

washtakiwa waachiwe huru. 

Wakili Didas Respicius, amesema hayo wakati akiwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa washtakiwa hao wamefikisha mwaka mmoja gerezani na upelelezi wa kesi inayowakabili bado haujakamilika. 

Wakili huyo ameyasema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Iman Mizizi kueleza upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. 

Didas amedai kuwa washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Juni 19, 2017 wakiwa na mashtaka ambayo yanadhaminika lakini wakiwa katika kuwasilisha maombi ya dhamana, walibadilishiwa mashtaka ambayo hayana dhamana. 

Amesema tangu mwaka jana hadi sasa upande wa mashtaka unadai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, kwamba kuwa kwa mujibu wa hati ya mashtaka washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo, mwaka 2013. 

Pamoja na hayo Wakili Mizizi amesema Katiba ndiyo inayotumika kutunga sheria na ndiyo iliyotumika kuwafunguliwa mashtaka washtakiwa .

Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Shaidi amesema amezingatia hoja zote na akashauri upande wa utetezi kupeleka maombi Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata maelekezo ya sheria ambazo zinalalamikiwa na zile zinazowafunga mikono. 

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 7, 2018 kwa ajili ya kutajwa. 

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola 22 milioni za Marekani.