Jumapili , 16th Jan , 2022

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla,amewaomba wahanga wa moto Soko la Karume kuwa watulivu, kwani inaundwa kamati ya kuchunguza chanzo cha moto katika Soko la Karume ambapo vyombo vyote ya ulinzi na usalama pamoja na Afisa Biashara Jiji na mkoa wataingia kwenye kamati hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akiwa Soko la Karume

Makalla ameyasema hayo leo Januari 16, 2022 baada ya kufika eneo la Karume Ilala Jijini Dar es salaam kujionea hali ya Soko la Karume ambalo limeteketea kwa moto alfajiri ya leo.

''Serikali itafanya jitihada ya kuhakikisha kwamba tunajua chanzo lakini pia tunakuja na suluhisho ya sisi kurejea katika kufanya biashara baada ya kupokea taarifa na maamuzi ya nini kifanyike katika soko hili,'' ameeleza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.

''Tuwaombe muwe watulivu. Majanga haya yanapotokea yanahitaji maneno ya faraja kama ambayo tunawapa, lazima tutafute njia mbadala ili maisha yaendelee," amesema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla.

''Si rahisi leo ukadhani kwamba baada ya hapa tutaacha tu kamati ifanye kazi, watu hawa walioko hapa lazima maisha yaendelee na ili maisha yaendelee ni maelekezo yangu kwamba Uongozi wa Jiji la Dar ukiongozwa na DC na Uongozi wa Soko, tuangalie namna ambavyo tunaweza kuwasaidia Wafanyabiashara hawa katika masoko ya jirani,'' ameongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla.