Jumanne , 13th Oct , 2015

Mkurugenzi wa taasisi inayojishughulisha na masuala ya utafiti (TWAWEZA) Aidan Eyakuze ametangaza rasmi mdahalo maalum utakao wakutanisha wagombea Uraisi wa vyama vitano tofauti

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam mkurugenzi huyo amesema mdahalo huu una lengo la kuwakutanisha wagombea Uraisi pekee na utashirikisha vyama vitano, lakini mpaka sasa ni vyama vitatu tu vilivyothibitisha uwepo wao katika mdahalo huo.

“Mpaka sasa vyama vilivyothibitisha uwepo wake ni ACT-Wazalendo, Chaumma na ADC, lakini tunaendelea kuwashawishi wagombea wa vyama vilivyobaki vya CCM na Chadema, ili nao waweze ksuhiriki katika tukio hili la kihistoria, tumetuma barua kwa vyama vyote na tunafuatilia ili waweze kuthibitisha ushiriki wao mapema iwezekananvyo,” alisema bwana Eyakuze.

Akijibu mapendekezo yaliyowahi kutolewa na mwenyekiti mwenza wa Ukawa bwana James Mbatia aliyewahi kukaririwa akisema Ukawa wangependa mdahalo wa vyama uwahusishe wenyeviti wa vyama na sio wagombea Uraisi, bwana Eyakuze alisema.

“Sisi tunataka wagombea husika waliothibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hatutabadilisha mfumo tuliojiwekea hata kidogo, na hatujakata tamaa bado tunaendelea kuwashawishi waweze kushiriki wananchi wawasikilize.”

Mdahalo huu unatarajiwa kuwa wenye mvutano mkali kupelekea hali ya kisiasa ilivyo nchini kwasasa na umeandaliwa chini ya muungano wa taasisi mbalimbali za CEE Roundtable, Tanzania Media Foundation (TMF), TWAWEZA na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA).