VIDEO: Mrema awahurumia wafungwa

Friday , 19th May , 2017

Mwenyekiti wa bodi ya Parole Taifa, Mh. Augustino Lytonga Mrema amefafanua na kusema sababu kubwa ya msongamano wa wafungwa Magerezani ni pamoja na wanachi kupenda kesi na visasi kwa kushindwa kumalizana mitaani, hivyo kuwataka kutoendekeza visasi .

Leo akifunguka kwenye East Africa Breakfast ya EA radio Mh. Mrema amesema kuwa wananchi wamekuwa sababu ya misongamano magerezani kwani kesi nyingine ni ndogo  za kuweza kumalizana nyumbani lakini wanaamua kukomoana kwa kupelekana polisi hadi kufikia kufungana.

Aidha Mh. Mrema ameongeza kwamba kuna wafungwa waliopo Magereza kwa kukosa watu wa kuwalipia faini hivyo ametoa nafasi kwa watu watakaoweza kufanikisha zoezi hilo waweze kuwasaidia  ndugu zao ikiwa ni pamoja na kuwaepusha na maradhi yapatikanayo kwenye msongamano wa magereza

"Kama Mume wako au mtoto wako amefungwa kwa kukosa faini unaruhusiwa kumlipia. ni vyema mkatumia nafasi ya sheria hii ili kuepusha msongamano magerezani. Lakini mnatakiwa kutambua kwamba kule siyo kuzuri na watu wanajifunza tabia mbaya na magonjwa mengi yanapatika kule, wasaidieni. Jukumu la kupunguza msongamano ni la wana ndugu"- alisema Mrema.

Pamoja na hayo Mh. Mrema ameongeza kuwa tayari ameshaliomba jeshi la polisi kuacha kuhangaika na mateja wasiojiweza kuwapeleka magereza bali wasaidiwe kwa kupelekwa vituo vya kuwasaidia waathirika wa dawa lakini pia wahakikishe wanaowapeleka magereza wawe mapapa wa dawa za kulevya ambao ni chanzo cha mateja nchini.

Mtazame Mh. Mrema hapa chini akifunguka kwa undani zaidi.