Ijumaa , 14th Mei , 2021

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Mei 14, 2021 ameshiriki swala ya Eid iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, na kuwasihi waumini wa dini ya Kiislamu kuhudhuria katika Baraza la Eid litalofanyika katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa

Akizungumza katika Swala hiyo Waziri Mkuu amewasihi Waislamu kujitokeza kwa wingi katika Baraza hilo ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, atakuwa mgeni rasmi.

“Niwasihi Waislamu wenzangu wote, tuhudhurie kwenye Baraza la Eid, mnatambua Rais wetu anakuja kwenye Baraza la Eid kwa mara kwanza ni vyema tukajitokeza kwa wingi kuja kupata neno kwa kiongozi wetu wa nchi,” amesema Mhe. Majaliwa.

Awali Mhe. Majaliwa amesema hawana budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwalinda hadi kufikia siku ya Eid, huku akisema kuwa ujumbe mahususi wa siku ya Eid utataolewa rasmi alasiri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufunga siku zote 30 na hatimaye leo tumeamka salama ni jambo la kumshukuru, tunatambua tutaendelea na siku 6, na mimi niwatakie kila kheri katika Sikukuu hii, huo ndio ujumbe wangu kwa leo," amesema Waziri Mkuu.