Jumamosi , 19th Mei , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amefunguka na kudai hayatambui makontena 20 yanayotaka kupigwa mnada na Mamlaka ya Mapato (TRA) kama ilivyoelezwa na wala hana 'document' zozote ofisini kwake zinazohusu masuala hayo.

Makonda ametoa kauli hiyo Mei 18, 2018 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake iliyopo Ilala Jijini Dar es Salaam kuhusiana na ushiriki wa Rais Dkt. John Magufuli kwenye mchezo wa leo wa kukabidhi kikombe cha Ligui Kuu Tanzania Bara kwa timu ya Simba ambayo inashuka kwenye dimba la Taifa na kukichapa na Kagera Sugar.

"Mimi sihusiki na lolote lile na wala sijui jambo lolote lile, mimi nimesoma habari hizo kwenye magazeti kama mlivyosoma nyie. Mimi sina 'document' yoyote yanayohusu mambo kama hayo kwa hiyo sijui lolote lile. Nimesikia na nitaendelea kusikia", amesema Makonda. 

Kauli hiyo Makonda imekuja baada ya hivi karibuni Mamlaka ya Mapato (TRA) kupitia Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA Richard Kayombo, kutangaza kusudio la kupiga mnada kontena 20 za Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa atashindwa kuzilipia ushuru na kuzichukua ndani ya siku 30 kuanzia Jumatatu.

Kontena hizo za Makonda ambazo zimesubiri utaratibu wa kuzitoa TRA kwa zaidi ya siku 90 zinazokubalika kwa mujibu wa sheria za kodi, zimesheheni samani za ndani na ofisini.