Jumapili , 13th Aug , 2017

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali italipa madeni yote ya Watumishi ambayo yamehakikiwa na kukutwa kuwa ni halali. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliyofanyika kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora na Rais Pombe Magufuli alisitisha malipo kwa sababu ya zoezi la kubaini watumishi hewa, sasa kazi hiyo imeshakamilika na yale yaliyobainika kuwa halali yatalipwa huku akiwataka Watumishi hao wafanye kazi ya kuwadumia wananchi kwa bidii.

"Hivi sasa tunadhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya watumishi, hakuna madeni ya matibabu, ya likizo au ya masomo. Kila mtumishi anaruhusiwa kujiendeleza, lakini ni lazima kwanza aandike barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuelezea nia yake na akikubaliwa, ndipo aanze kutuma maombi kwenye vyuo. Mtumishi akiamua kuomba chuoni moja kwa moja ndipo alete madai yale, hatapewa chochote kwa sababu ni nje ya utaratibu," alisema Majaliwa.

Pamoja na hayo, Waziri Majaliwa amesema serikali imeondoa utaratibu wa Mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja au cheo ndipo aanze kupata stahiki zake mpya.

"Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo. Mimi nimekuwa kwenye utumishi wa umma kwa muda mrefu, sijawahi kuona mtu anaandikiwa barua ya kupandishwa daraja halafu anakataa. Kikubwa ni kwa maafisa utumishi kuona kama kuna Watumishi wanastahili kupandishwa madaraja, watume taarifa zao mapema kabla ya tarehe 10 ya kila mwezi ili waingizwe kwenye mfumo huo. kisha wawaandikie barua za kuwajulisha wahusika. Hata barua ikichelewa kumfikia mtumishi, mshahara wake hautachelewa na kwa njia hii tutaepuka kuweka madeni yasiyo na tija", alisema Waziri Majaliwa.

Kwa upande mwingine, Majaliwa amewataka Watumishi hao kuwahudumia watanzania bila kujali hali zao kwa kuwa serikali haitamvumilia mtu mdanganyifu, mzembe, asiye muadilifu na mla rushwa na endapo atabainika hatoweza kuundiwa tume kwa madai tume zao zinamaliza fedha, bali wakiwa na ushahidi wa kutosha watamalizana naye hapo hapo.