Alhamisi , 29th Sep , 2022

Wadau wa maendeleo ya jamii wameiomba serikali kuandaa sera na baadae sheria rasmi kuhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuruhusiwa kurejea shuleni, ili kuepukana na mkanganyiko miaka ya ijayo.

Mwanafunzi mwenye ujauzito

Hayo yameelezwa wakati wa kongamano lililohusisha wanafunzi, wadau wa maendeleo ya jamii na mabinti wengine kutoka maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, huku wakikiri kuwa bado elimu ya kutosha haijatolewa kwa jamii kuhusu namna binti anavyoweza kurejea shule baada ya kupata ujauzito.

Kwa upande wao wanafunzi wa kike, ambao ndio wahanga wa kubwa  wa mimba za utoto na ndoa za utotoni, wamebainisha kuwa hali ngumu ya maisha imekuwa kishawishi kikubwa kwa baadhi ya mabinti kupata ujauzito, huku wakiomba kuendelea kupewa elimu zaidi.

"Ni vyema serikali ikatengeneza sera ambayo baadaye itakuwa sheria, kwa wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa masomoni, kupewa nafasi ya kurejea tena shule, japo bado elimu haijatolewa vya kutosha juu ya namna ya kurejea shule baada ya kupata ujauzito."-Amesema katibu mtendaji wa shirika la Voice of encouragement Tanzania

Nao viongozi wa dini wanatoa wito kwa jamii kuzingatia mafundisho ya dini zao, na kurejea kwenye maadili yetu ya Kitanzania na kuacha kuiga tamaduni za kigeni zinazosababisha kuongezeka kwa vitengo vilivyokinyume na maadili yetu.

"Watu wamekosa maadili siku hizi, hata mavazi wanayovaa pia yanachochea vitendo vya unyanyasaji kwa wasichana kuongezeka nchini."- Amesema Mchungaji Daudi Zacharia