Ijumaa , 2nd Dec , 2022

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima, amezitaka Halmashauri zote mkoani humo kupunguza vikao visivyo vya lazima na badala yake kuongeza nguvu katika kupeleka elimu ya kujikinga na VVU kwa jamii kwani kasi ya maambukizi ni kubwa katika mkoa huo.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima

RC Malima amesema takwimu zinaonesha mkoa huo upo kwenye hatari zaidi ya maambukizi kwa mujibu wa takwimu za kitaifa hivyo watendaji wa serikali na taasisi mbalimbali zinatakiwa kuelekeza nguvu zaidi katika kuelimisha jamii ili wawe katika kiwango cha chini kufikia 2030.

"Kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kitaifa ni asilimia 4.7 na Mwanza ni asilimia 7.2 hii ni ishara kwamba Mwanza tuna jitihada kubwa za kufanya kwa sababu maambukizi yetu katika miaka hii mitano ya tathmini iliyofanywa maambukizi yetu bado ni makubwa kuliko wastani wa kitaifa, mapambano hayo hatuwezi kuyashinda kwa kuongeza vikao bali kwa kuongeza uwajibikaji wa kupeleka elimu ya kupambana na maambukizi huko kwa wananchi" amesema RC Malima.

Kwa upande wake Insp. Jovitha Ezekiel kutoka kitengo cha Polisi jamii mkoani humo akatoa wito wa kuripoti mapema kwa mtu anayetendewa vitendo vya ukatili.

"Tunashauri mtu kama amefanyiwa kitendo cha ukatili labda amebakwa atoe taarifa kituo cha polisi ndani ya saa 72 unakuta mtu aliyemfanyia ukatili labda afya yake siyo nzuri ina maana akifika ndani ya masaa 72 atapata PF3 atahudumiwa na watu wa dawati waliopata mafunzo maalum na kufikishwa hospitali kwa haraka apate matibabu" amesema Inspekta Jovitha