Jumamosi , 3rd Dec , 2022

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na mbunge wa Mtama Nape Nnauye amesema yeye ni miongoni mwa watu wanaopiga debe Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuchaguliwa katika uchaguzi wa 2025 hadi 2030 ili amalizie kazi ambayo ameianza

Nape ametoa kauli hiyo katika mjadala uliofanyika kwa njia ya mtandao (Zoom) ukiwakutanisha wadau mbalimbali kuhusu maendeleo ya mikoa ya kusini 

"Mimi ni katika wale wanaopiga debe wazi kabisa bila aibu, kwamba mama anastahili kuongezewa muda, akimaliza 2025 tumchague tena hadi 2030, tuna hakika akifika huko atakuwa ametufanyia kazi nzuri kwa mujibu wa katiba yetu atakuwa ndio wakati wa kupumzika" 

Aidha Nape amesema Rais Samia ameacha alama na amerudisha matumaini kwa watu waliokuwa wamepoteza matumaini 

"Rais Samia amerudisha matumaini mahali ambapo watu walianza kukata tamaa, amerudisha furaha mahali ambapo watu walianza kuvunjika moyo, amerudisha upendo mahali ambapo kulikuwa na chuki pengine, na ametuleta pamoja kama watanzania, jambo hili ni kubwa sana"

Kuhusu mikoa ya Lindi na Mtwara na maendeleo yake Nape amesema mikoa hiyo imeanza kupiga hatua kmaendeleo tofauti na watu wanavyoifikiria

"Mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa ambayo kwa muda fulani hivi ilikuwa nyuma kimaendeleo na ni kwa sababu za kihistoria"

"Mimi jimbo langu la Mtama kwa miaka mitano tulikuwa tunapata fedha kidogo sana za ujenzi wa barabara, baada ya kuanzishwa kwa TARURA haikutengewa fedha ila Rais Samia alivyokuja akatenga fedha bungeni zikaja milioni 500 kwa majimbo yote"

Aidha mbunge wa Lindi Hamida Abdallah amesema serikali ya awamu ya sita imekuwa na kasi kubwa ya maendeleo ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama 

"Kwa kipindi hiki cha awamu ya sita tumeona kasi ya maendeleo inakuja kwa kasi kubwa sana, Lindi kulikuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji safi na salama lakini serikali imeweka nguvu wametuoatia fedha zaidi ya bilioni 9" 

"Eneo ambalo limesahaulika ni Lindi mjini lakini ukiangalia namna ambavyo mji ulikuwa na sasa hivi ulivyo kumekuwa na mabadiliko makubwa, kumekuwa na barabara za lami, taa za barabarani na serikali imetuhakikishia fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati"

Kuhusu uwekezaji katika gesi Mkurugenzi Mkuu TPDC James Mataragio amesema ujio wa mradi wa LNG utaongeza pato la taifa na kukuza uchumi wa watanzania huku akiweka wazi kuwa tayari wananchi hususani mikoa ya kusini wameanza kuona matunda ya gesi 

"Mradi wa gesi wa LNG tunategemea utaleta mtaji wa kiasi cha dola za kimarekani bilioni 40, ni fedha nyingi sana na hivi karibuni mradi huu umekuwa namba moja kwa nchi hizi za kusini mwa Afrika" 

"Tayari nchi inafaidi uchumi wa gesi, mpaka leo tunapoongea asilimia 70 ya umeme wote unatumia gesi asilia, kwamba ule umeme unaozalishwa unatumia gesi asilia, ni kwamba tayari wananchi wa mikoa ya kusini wanafaidi matunda ya gesi" 

Mjadala huo pia umehudhuriwa na Mrajisi wa vyama vya ushirika na mtendaji Mkuu tume ya maendeleo ya ushirika Dkt Benson Ndiege na Mkurugenzi wa bodi ya Korosho Francis Alfred,