Jumatatu , 16th Mei , 2022

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewakaribisha Rasmi Tanzania, Ujumbe wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Sekta Binafsi kutoka nchini Ufaransa MEDEF pamoja na Taasisi ya Biashara ya Ufaransa Business France, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Mei, 2022.

Akizungumza na Wajumbe hao ambao kati yao ni Makampuni 41 pamoja na Wajumbe 50, Rais Samia amesema huo ni mwanzo mzuri kwa makampuni hayo kuja kuangalia fursa mbalimbali za kibiashara pamoja na uwekezaji zinazopatikana nchini.

Rais Samia amesema kwamba Makampuni hayo yamekuja kutokana na Ziara yake ya Kikazi aliyoifanya nchini Ufaransa ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na kuzungumza na Rais wa nchi hio Emmanuel Macron pamoja na kushuhudia utiaji Saini wa Mikataba mbalimbali ya kibiashara kati ya Tanzania na Ufaransa.

Katika Kikao chake na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mhe. Rais Samia amesema walikubaliana mambo kadhaa ikiwepo kuendeleza ushirikiano wa siku nyingi baina ya nchi hizi mbili.

Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania ni Sehemu ya salama ya Uwekezaji na atahakikisha anaondoa vikwazo vyote katika uwekezaji na ufanyaji wa biashara nchini.

Mhe. Rais Samia amewakaribisha Wajumbe hao kuitembelea Bandari ya Dar es Salaam ili kujionea ufanisi wake, vivutio mbalimbali vya Utalii kama Mlima mrefu kuliko yote Barani Afrika Mlima Kilimanjaro, Mbuga ya Wanyama Serengeti pamoja na Kisiwa cha Zanzibar kwasababu wamepata fursa ya kuja nchini.  

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti ambaye ni Kiongozi wa Ujumbe huo wa Wafanyabiashara kutoka Ufaransa Bw. Gerard Wolf amesema kuwa Wameitikia wito alioutoa Mhe. Rais Samia kwa wao kuhakikisha wanakuja nchini Tanzania mapema mara baada ya ziara yake ya Kikazi nchini Ufaransa. 

Bw. Wolf amesema kuwa katika Ujumbe waliokuja nao nchini, yapo Makampuni 41, na Wajumbe 50 kwa ajili ya kuja kuangalia fursa mbalimbali za Uwekezaji na kufanya Biashara nchini Tanzania.

Bw. Wolf amesema wamekuja Tanzania ajili ya Biashara na tayari makampuni pamoja na Wafanyabiashara kutoka Ufaransa yanafanya vizuri na wanategemea kwenda mbali zaidi katika Uwekezaji wao hasa 
sekta ya Nishati jadidifu, Tehama, sekta mbalimbali za kiuchumi. 

Amebanisha kuwa hata katika kipindi cha janga la ugonjwa wa Uviko 19, makampuni na wafanyabiashara wa Ufaransa hawakuondoka nchini ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kufanya kazi kwa bidi kwa kujali muda na Mafanikio ya pande zote.