Jumatano , 27th Sep , 2017

Wananchi jamii ya Wahadzabe wanaoishi kwa maisha ya asili ya kula nyama, asali  na matunda huku wakilala nyumba za nyasi  wameomba serikali kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF awamu ya tatu kuwajengea nyumba imara ili waache

maisha ya kuhamahama wakati wa mvua.

Mwenyekiti jamii ya Wahadzabe kutoka kijiji cha Endamaghan tarafa ya Eyadi wilayani Karatu, Julius Ndaya amesema wanaishukuru serikali  kupitia mpango wa TASAF kuwasaidia kumiliki ardhi, pesa za kununua mahindi ya chakula na mahitaji ya watoto wao wa shule za msingi na serikali.

Amesema pamoja na msaada huo wameona ipo haja sasa ya kuishi maisha ya kuwa na  nyumba bora japo hawataziacha nyumba za asili watakazozijenga pembeni mwa nyumba hizo imara ili kuenzi mila na tamaduni zao.

Pia wameomba kusaidiwa mradi wa mizinga ya nyuki kwa ajili ya kuweza kuvuna asali pasipo kutembea umbali mrefu kama ilivyo sasa na kuweza kutunza mazingira waliyopewa na serikali.

"Nyumba zetu siyo za kudumu kwa sababu tunahama hama kutafuta chakula kama matunda, asali na mambo mengine. Lakini hata wakati wa kurudi huwa tunarudi kwenye nyumba zetu kwa sababu tunahama kwa kuzunguka pori. Lakini tukipatiwa nyumba imara tutatulia sehemu moja".

Mkurugenzi wa mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF,  Amadeus Kamagenge amesema mpaka sasa wametumia zaidi ya shilingi bilioni 36 kusaidia watu milioni sita nchini na huku wakitilia mkazo suala la kuwekeza afya ya mtoto na lishe.