Jumatano , 23rd Jun , 2021

Mwanamitindo na Muanzilishi wa Taasisi ya Flaviana Matata FMF, Flaviana Matata amesema hana mpango wakufanya biashara ambayo haigusi wala kurudisha jamii kwani hata katika biashara zake za sasa zinarudisha kwa jamii.

Mwanamitindo na Muanzilishi wa Taasisi ya Flaviana Matata FMF, Flaviana Matata

Mwanamitindo huyo wa Kimataifa amesema hayo leo katika mahojiano yake na kipindi cha Supa Breakfast ambapo amesema anashirikiana na kampeni ya Namthamini ya East Africa Television na East Africa Radio kwa sababu taasisi ya FMF imejikita katika shughuli za kumsaidia na kumuwezesha binti wa kike.

 

“Nilisema sitaki nifanye biashara ambayo haigusi jamii kwa namna yoyote, sisi tunafundisha wasichana namna ya kutengeneza kucha, kwenye taulo za kike 10% inayopatikana tunarudisha kwa jamii, hata biashara tutazoanzisha lazima ziwe zinarudisha kwa jamii,” amesema Flaviana.

Akielezea safari yake mpaka kufika kwenye uwanamitindo Flaviana amekiri kuwa hakutaka kushiriki katika shindano la Miss Universe bali watu wachache walimsukuma akiwemo marehemu Ruge Mutahaba huu akiweka wazi kuwa hana mpango wa kuigiza.

“Miss Universe sikutaka kufanya nilikuwa tomboy, sijui kutembelea viatu ila Marehemu Ruge alinisukuma na dada Irene akanifundisha kuvitembelea, nilivoshinda Miss Universe watu walishangaa kwa sababu walijua nipo kujifurahisha,” amesema Flaviana.

Aidha, Flaviana amesema bado ipo changamoto ya mfumo dume hususan pale viongozi wanavyochaguliwa huku akigusia kelele zilizokuwepo pindi Mhe. Jokate Mwegelo alivyoteuliwa kuwa kiongozi.

“Mfumo dume bado upo, changamoto bado zipo unaona viongozi wa aina fulani wakichaguliwa watu wanaongea, nakumbuka Jokate alivyochaguliwa kulikuwa na kelele nyingi, hata kama alikosea huko nyuma nani hajawahi kukosea kwenye maisha yake ?,” alihoji Flaviana.