Ijumaa , 24th Jul , 2020

Mwenyekiti wa chama cha UDP Mzee John Cheyo amesema kuwa kwa muonekano Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa alikuwa ni mkali lakini ndani ya moyo wake alikuwa ni mwenye huruma, huku akikumbuka namna alivyomkuta akilia baada ya gari lake kugonga watu jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa chama cha UDP, Mzee John Cheyo.

Mzee Cheyo ametoa kauli hiyo hii leo Julai 24, 2020, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio.

"Nakumbuka mwaka 2000 tukiwa kwenye kampeni Mwanza,  gari lake liligonga watu na kwa bahati mbaya walifariki, nilienda kumfariji nikamkuta anatoa machozi kuwalilia wale watu, alikuwa ni mkali lakini alikuwa na moyo wa kuhurumia watu" amesema Mzee Cheyo.

Aidha Mzee Cheyo ameongeza kuwa, "Kwangu Mkapa ni kiongozi aliyekuwa na busara, kama kulikuwa na mtu ambaye alikuwa anatoa hotuba mpaka zina kusisimua na kama kulikuwa na kiongozi aliyetumia lugha ya Kiingereza vizuri ni Mzee Mkapa".

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo Julai 24, 2020, katika moja ya Hospitali zilizopo jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.