Jumatano , 20th Oct , 2021

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Tanzania Samson Mwela amesema siku ya kwanza ya Kongamano la Tano la Mkutano Mkuu wa Tehama 2021 imekuwa yenye mafanikio makubwa baada ya wawekezaji mbalimbali kukubali kushirikiana na serikali katika kukuza Tehama nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Tanzania Samson Mwela (kushoto) akifanya mahojiano na Irene Tillya,

Mwela ameyasema hayo jioni ya leo Oktoba 20, 2021, kwenye mahojiano na EATVSaa1 yaliyoruka mojamoja kutokea Ukumbi wa Simba ndani ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), ambapo amesema huu ni mwanzo tu mengi zaidi yakuja.

‘’Kikubwa ambacho leo tumefanya ni mkutano na wawekezaji ‘Investors Round Table’ na hili jambo limeonekana #LIVE duniani kote, kiukweli kumekuwa na mafanikio makubwa sana kwasababu wameonesha nia ya kushirikiana na serikali kwenye kukuza Tehama nchini,’’ amesema Samson Mwela, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Tanzania Samson Mwela (kushoto) akiwa kwenye mkutano.

Aidha Mwela ameongeza kuwa, ‘’Siku ya leo imekuwa na mafanikio sana mwitikio wa watu umekuwa mkubwa sana, tunatarajia kesho watu watazidi kujitokeza zaidi kwasababu tunajadili masuala ya msingi hususani taifa na uchumi wa kidijitali jinsi gani watu watatumia Teknolojia kujiletea maendeleo,’’.

Kuhusu ujenzi wa taifa la kidijitali Mwela ameweka wazi kuwa, ‘’Tunafahamu suala la kodi linaonekana ni changamoto na limeongelewa, sasa jinsi gani taifa linufaike kupitia Tehama kwenye kukusanya kodi na tumekubaliana, jambo la msingi sasa ni kuangalia tu ni namna gani mifumo yetu itatumika,’’.

Washiriki mbalimbali wa mkutano wakiwa kwenye Ukumbi wa Simba ndani ya AICC.

Pia Mwela amedokeza kuhusu mjadala utakaoendelea kesho kwenye mkutano kwa kusema, ‘’Kesho tutaangalia uchumi wa kidijitali, jamii ya kidijitali na utawala wa kidijitali kwahiyo haya yote ni masuala ya msingi leo tumeanza tu ila kesho tutaendelea kwa upana wake,’’.