Jumamosi , 28th Jan , 2023

Mwili wa Mtanzania Nemes Tarimo, aliyefia vitani nchini Ukraine, wakati akilitumikia jeshi la nchi ya Urusi, umezikwa hii leo Januari 28, 2023, Tukuyu mkoani Mbeya.

Kaburi la Nemes Tarimo

Nemes alikwenda nchini Urusi kwa ajili ya masomo ambapo baadaye alikutwa na hatia ya uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 7 na umauti ulimfika Oktoba 24 mwaka jana akiwa vitani.

Januari 24, 2023, Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Stergomena Tax, alisema kuwa Mtanzania huyo alikuwepo nchini Urusi kwa ajili ya masomo na alijiunga na chuo cha Moscow Technology Pro mwaka 2020 kwa masomo ya shahada ya uzamili katika fani ya Business Informatics.

Dkt. Tax aliongeza kuwa taarifa walizozipokea ni kwamba mwezi Machi 2022 Mtanzania huyo alikuhumiwa kifungo cha miaka saba gerezani kwa mujibu wa sheria za Urusi kwa vitendo vya uhalifu.

Na kwamba akiwa gerezani alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi cha kijeshi kilichopo nchini humo kinachofahamika kama Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha lakini pia kwa ahadi ya kuachiwa huru mara baada ya vita na alikubali kujiunga na kikundi hicho.