Jumapili , 17th Oct , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema ziara anazofanya nchi mbalimbali zinafaida kubwa kwa nchi hivyo wananchi wasibeze kwani nchi inafunguka na wafanyabiashara sasa wanaweza kuunza ndani na nje ya nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

''Tukizunguka msisema mama anazunguka tu, sitazunguka bila sababu. Nilishacheza vyakutosha kwenye nchi nyingi duniani sasa hivi kazi ni moja tu kuzunguka kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania,'' amesema Rais Samia Suluhu, leo mkoani Arusha wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara.

Katika hatua nyingine ameeleza faida ya zaira alizofanya nchi za nje. ''Ziara nilizokuwa nafanya kwenye nchi jirani madhumuni ilikuwa kuondoa vikwazo vilivyokuwepo, kunyoosha njia ili wafanyabiashara wetu waweze kuuza ndani waweze kuuza nje, tumeondoa vikwazo na Kenya nimeambiwa biashara imekuwa mara 6 kuliko wakati wa vikwazo''.

Aidha amesema hatoogopa kuchukua mikopo ambayo itakuwa na lengo la kusaidia taifa huku akiweka wazi kuwa ile mikopo chechefu hatoichukua.

''Nataka niwaahidi watanzania nitaangalia mikopo yenye unafuu kwa nchi yetu, inayoleta faida kwa nchi yetu, hiyo nitaichukua, mikopo chechefu sitaichukua, lakini inayotusogeza watanzania hiyo sitaogopa nitaichukua,'' amesema Rais Samia Suluhu.