
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein (katikati)
Mama Mwanamwema Shein ameyasema hayo leo Ikulu ndogo Chake Chake Pemba katika mkutano kati yake na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wa Majimbo ya Pemba pamoja na wale wa Viti Maalum.
Mama Shein, amewataka viongozi hao kutambua kuwa nyazifa zao ni za ulezi na usimamizi wa jamii wanayoizunguka ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza vijana kukimbilia katika kazi za halali zitakazowapatia kipato kwani serikali haina ajira za kutosha kwa wote wanaohitaji.
“Kwa kuwa mimi ni mzazi, naguswa sana na hatma ya vijana wetu kuendelea kudanganywa na kudanganyika hivyo tuendelee kuwaelimisha katika majimbo yetu kuwa wakatae kutumika katika vitendo vinavyoweza kuvuruga amani, wajue kuwa uchaguzi umekwisha”, alisema Mama Shein.
Aidha, aliwataka viongozi hao kuwaelimisha vijana juu ya madhara ya utumiaji wa dawa za kulevya na kuwataka vijana walioko mashuleni kuongeza bidii katika masomo yao kwani nchi hii itajengwa na wananchi wenyewe hasa vijana wenye maarifa na ujuzi.