Ijumaa , 14th Mei , 2021

Wakazi wa kata tatu za Katoro, Kyamulaile na Ruhunga zilizoko katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wameiomba serikali kuwaondolea kero ya kuvuka kwa mitumbwi katika eneo la Katokoro, iliyosababishwa na barabara yao kuvunjika na kujaa maji, tangu msimu wa mvua 2019.

Wakazi mbalimbali wakiwa kwenye kivuko

Wakizungumzia kero hiyo wakazi hao wamesema kuwa ni takriban miaka mitatu sasa wanateseka na kwamba tatizo hilo limesababisha gharama za usafiri na usafirishaji kupanda.

Mmoja wa wananchi hao Imani Abeid mkazi wa kijiji Katokoro amesema kuwa zamani walitumia shilingi 1,000 kutoka kijiji hicho kwenda Katoro na kurudi, lakini kwa sasa wanatumia shilingi 6,000 kwenda na kurudi.

"Ukitoka hapa Katokoro kwenda Katoro utapanda bodaboda ulipe shilingi 1,000 na pia utalipa shilingi 1,000 ili uvushwe kwa mtumbwi, ukishavuka kwa kuwa hata upande wa pili hakuna magari utapanda tena bodaboda hadi Katoro kwa kulipa shilingi 1,000 hapo jumla ni shilingi 3,000 ambayo kwenda na kurudi ni shilingi 6,000" amesema Abeid.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na changamoto hiyo meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini - TARURA- katika halmashauri ya wilaya hiyo mhandisi Ally Maziku amesema kuwa serikali imeanza kulifanyia kazi suala hilo, na kuwataka wananchi kuwa na subira.

"Mkandarasi aitwaye Rumanyika alikuwa tayari kazini, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha amesitisha kazi kwa muda, lakini nina imani kufikia Septemba mwaka huu kazi ya kutengeneza barabara katika eneo hilo itakamilika kwa mujibu wa mkataba" amesema mhandisi Maziku.

Kwa upande wake mratibu wa TARURA Mkoa wa Kagera mhandisi Avity Theodory amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto za ubovu wa barabara katika maeneo korofi wanalazimika kuomba fedha nje ya bajeti.

"Bajeti ya Tarura mkoa ni shilingi bilioni 9.3,  tumeomba fedha nje ya bajeti hiyo tukapata shilingi milioni 485 kwa ajili ya kutengeneza eneo hilo la Katokoro, lkn pia tumepata shilingi milioni 80 kwa ajili ya matengenezo ya barabara eneo la Rwabwere Karagwe" amesema mhandisi Theodory.

Jumla ya mitumbwi 33 inatumika kuvusha wananchi katika eneo hilo la Katokoro.