Ijumaa , 23rd Aug , 2019

Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaulembo, amesema hana mpango wa kumng'oa Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, kwa kuonesha nia ya kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Meya Chaulembo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Breakfast cha East Africa Radio, wakati akijibu swali juu ya mpango wake wa kugombea kiti cha Ubunge na kumng'oa Mbunge wa sasa wa jimbo la Temeke.

"Kuhusu mimi kutaka kuwa Mbunge, Watanzania wajue tunao wabunge wawili ambao ni Mtolea na Mangungu, mimi sijawahi kutamka kwamba nitagombea Ubunge, ila nimeonesha nia ya kwenda kugombea Usheikh wa Kata, na nimesikia fomu zimeshaanza kutoka nimwambie tu Sheikh wangu akae mkao wa kula, ila haya masuala ya Ubunge yanaletwa na Mungu." amesema Chaulembo.

Kuhusiana na Wilaya ya Temeke kuwa miongoni mwa Wilaya kinara kwa uchafu, Chaulembo amesema moja ya sababu ni Temeke kuwa na wakazi wengi.

"Unajua moja ya sababu Temeke kuongoza kwenye suala la uchafu, ikiwa tofauti na maeneo kama Arusha, Moshi au Iringa, usichokijua ni kwamba idadi ya wakazi wa Iringa ni sawa na Kata 1 Temeke, kingine Temeke lazima ujue ina mkusanyiko wa watu wa Mikoa mingi sana." amesema Chaulembo.