Jumapili , 10th Oct , 2021

Waziri wa Fedha na Mipango Tanzania Dk. Mwigulu Nchemba ameweka wazi mpango wa matumizi ya fedha za mkopo wa Shilingi Trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo kwa kiasi kikubwa zitatumika kwenye miradi ya afya na elimu.

Waziri wa Fedha na Mipango Tanzania Dk. Mwigulu Nchemba

Dk. Nchemba amesema hayo leo Jumapili Oktoba 10, 2021 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.

''Kutokana na maelekezo yako Mhe. Rais, tunajenga madarasa elfu 15 kwa mpigo kwenye shule zetu za sekondari. Tunakwenda kujenga madarasa elfu 3 kwa mpigo kwenye shule za msingi. Tunaenda kununua madawati laki 462,795 ili kuondoa mbanano wa watoto,'' ameeleza Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha.

Kwa upande wa elimu ngazi ya vyuo Dk. Mwigulu amesema kuwa, ''Tunakwenda kumalizia shule za VETA katika mikoa 6 zilizopo kwenye hatuza za mwisho na 26 zilizokwama kwa muda mrefu. Tunajenga madarasa katika vyuo 17 vya ualimu na kuchapisha vitabu elfu 10,812 vya nukta nundu ili kuwaepusha wenzetu wenye matatizo ya kuona kuchangia vitabu''.

Kwenye upande wa afya Dk. Mwigulu ameeleza kuwa,''Mhe Rais tunakwenda kununua Digital X-Ray 85 kwa mpigo, pia tunakwenda kununua CT scan machine 29 kwa mpigo kwenye hospitali za mikoa yote ili watu wetu sasa wasihangaike kufuata huduma hii kwenye hospitali chache''.

Zaidi tazama video hapo chini