Jumatano , 14th Aug , 2019

Kesi ya kupinga kuvuliwa ubunge iliyofunguliwa na Tundu Lissu inatarajiwa kuanza kusikilizwa kesho, baada ya Mahakama kuu ya Tanzania kutoa wito ya kuwataka wahusika katika shauri hilo kufika mahakamani kesho.

Lissu amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake wakili, Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo ambapo katika kesi hiyo Lissu anamshtaki Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Kwa mujibu wa maombi namba 18 ya mwaka 2019, Lissu ameiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe taarifa yake ya kumvua ubunge.

Aidha Lissu ameiomba mahakama impe kibali afungue shauri ili mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa Mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa CCM.