Ijumaa , 2nd Dec , 2022

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limesema kwamba bado ukame unaendelea kuyakumba mabwawa ya uzalishaji wa umeme yanayotegemewa na shirika hilo licha ya uwepo wa mvua kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande

Kauli hiyo imetolewa hii leo Desemba 02, 2022, jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Maharage Chande, wakati akitoa taarifa ya hali ya umeme nchini.

"Kwa kipindi cha wiki moja tangu tarehe 23 katika mabwawa yetu hatujaona mtiririko wa maji wa kutosha kuweza kuongeza uzalishaji wa umeme," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO

Aidha Mkurugenzi huo ameongeza kuwa "Ni kweli baadhi ya maeneo tumeanza kuona mvua zikinyesha, lakini yale maeneo muhimu yanayodaka maji kwenye mabwawa yetu bado mvua hazijaanza kunyesha, mikakati yetu bado imejikita kuongeza nguvu katika uzalishaji wa gesi, ile sababu ya ukame tuliyoizungumza bado ipo unaweza ukaona mvua imenyesha Mkuranga ukasema mbona Mkuranga inanyesha, ni ndiyo lakini hainyeshi kwenye mabwawa yetu," amesema Mkurugenzi huyo.

Akizungumzia suala la mradi wa Kinyerezi 1 Extension amesema, "Tulisema kwamba kituo cha Kinyerezi namba 1 extension tulisema tutapata megawatt 60 tukifika wiki hii ya kwanza ya Desemba, mpaka saas tunapata Mg 65, vimebaki vitu vichchewiki inayokuja tutavimaliza ili tupate megawatt 90 Desemba mwishoni,".