Jumatano , 16th Mei , 2018

Korea Kaskazini imetishia kuufuta mkutano kati ya kiongozi wake Kim Jong-un na Rais wa Marekani Donald Trump iwapo Marekani itaendelea kusisitiza kwamba taifa hilo ni lazima liharibu au kusalimisha silaha zake za nyuklia.

Mkutano huo ambao umesubiriwa kwa hamu kati ya Rais Trump Bw. Kim unatarajiwa kufanyika mnamo 12 Juni, hayo yamejiri baada ya Korea Kaskazini kusema imejitolea kuhakikisha silaha za nyuklia zinaondolewa katika rasi ya Korea.

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini KCNA limemnukuu naibu waziri wa mambo ya nje Kim Kye-gwan akisema iwapo Marekani "itatubana na kusisitiza kwamba ni lazima tusalimishe bila masharti silaha zetu za nyuklia basi hatutakuwa tena na hamu ya kushiriki mazungumzo hayo na itatulazimu kutafakari upya iwapo tutakubali mkutano unaotarajiwa kufanyika karibuni”. Amesema Kye-gwan.

Maafisa wa ngazi ya juu wa mataifa hayo walitarajiwa kukutana katika eneo la mpakani ambapo majeshi hayaruhusiwi lakini Korea Kaskazini ilijiondoa ikisema imekerwa na mazoezi makubwa ya kijeshi yanayoandaliwa kati ya Korea Kusini na Marekani.